Sunday, March 4, 2018

KATIBU MKUU WA CHADEMA AWAONGOZA MAKAMANDA WENZAKE KWENDA KURIPOTI POLISI

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na viongozi wengine wa chama hicho wameripoti Kituo Kikuu cha Polisi leo asubuhi Machi 5, 2018.
Tokeo la picha la CHADEMA
Februari 27, 2018 viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye leo hayupo kwa maelezo kuwa ni mgonjwa, walifika kituoni hapo na kuhojiwa kwa takribani saa tano, kisha kuachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena leo.

Viongozi hao wakiongozwa na Dk Mashinji ambaye Februari 27, 2018 hakufika kuhojiwa kutokana na kuwa nje ya nchi, mpaka saa 2:15 asubuhi walikuwa wamewasili wote kituoni hapo.

Mbali na Mashinji, viongozi wengine waliofika kituoni ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Pia, wamo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Viongozi hao wameambatana na wakili Frederick Kihwelo na Alex Massaba pamoja na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Massaba amesema kuwa Mbowe hatoweza kufika kwa kuwa ni mgonjwa.

Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.

Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.

No comments: